Featured

Karibu waandishigroup

This is the post excerpt.

Advertisements

Sisi ni kikundi cha waandishi.

Lengo kuu ni kuwezesha watu kuandika mambo chanya katika maisha. Tutafundisha watu wanaopenda kujifunza kuandika. Tutawapa nafasi ya kuweka Makala zao katika ukurasa wetu. Uzoefu wa waanzilishi wa kundi hili umekuwa ni kuhariri Makala mbali mbali zinazochapwa katika mitandao ya kijamii pamoja na busati aina tofauti.

Haijawahi kuwa kazi rahisi kuandika. Hapa tutakupa msaada. Tutaweka Makala za kukusaidia uweze kuandika, na pia tutaandika Makala zinazohusu Nyanja nyingi, tutaeleza aina na mitindo inayotumika na mbinu mbali mbali za uandishi.

Hivyo, kikubwa utakachokipata kwetu ni kujifunza kuandika na kuelimika na Makala mbali mbali. Kuna usemi usemao  “kila mtu anatembea na kitabu / vitabu moyoni mwake”. Kitabu cha maisha, kitabu cha kazi, kitabu cha utaalamu, kitabu cha hadithi, pia unazo Makala nzuri sana. Kazi yetu sisi ni kuwa pamoja nawe uweze kuzitoa. kama unadhani hauna cha kuandika tutakupa. Karibu sana kwenye busati hili.

Utaweza kushiriki nasi kwa kutoa mawazo, kutuandikia, kutumia uwanja wetu kutuma Makala yako na kuwa mwanachama ikiwa utafikia malengo tutakayokupangia. Tutaangalia na kuhakiki ni ya kwako halisi. Tumeweka vizuri utaratibu utakaotumia ili iwe rahisi kwako kuweza kushiriki. Endelea kututembelea

Ni makusudio yetu kuibua wenye vipaji vya uandishi na wanaojifunza kazi hiyo yenye manufaa makubwa kwao, kwa jamii ya watanzania.

post

‘Kifungu cha maneno’ sehemu muhimu ya uandishi

Kuandika kifungu cha maneno kunabaki sehemu muhimu sana ya uandishi. Kifugu cha maneno kinakaa kama kibebeo cha mawazo kwenye insha au maandiko mbali mbali. Kifungu cha maneno kinaweza kuwa cha namna nyingi kuweza kuwasaidia wasomaji kupangilia mawazo uliyowasilisha.

Urefu wa kifungu cha maneno

ndio, ni kweli kwamba kifungu cha maneno kinaweza kuwa na urefu wowote. Inaweza kuwa  sentensi mbili au tatu ndefu. Mara nyingi kwenye gazeti au jarida wanapenda kutumia sentensi ndefu 1-3. Kwenye vitabu inaweza kuwa ndefu zaidi.

 Haijalishi kuwa ni urefu gani unaweza kuandika, unaweza kuandika kifungu cha kwanza kirefu, kifungu cha pili kifupi, na cha tatu kirefu ili kumpa anayesoma nafasi ya kupumzika.

Kutenganisha mawazo

Ni vyema kila wazo liwe na kifungu chake cha maneno. Kwa kawaida kifungu cha maneno kinagawanyika sehemu tatu. Sehemu ya kwanza ni wazo lenyewe sehemu ya pili ni maelezo sehemu ya tatu ni majumuisho. Kwa hiyo kila kimoja kinaweza kuwa na sentensi yake. Na mara nyingi sentensi ya kwanza ndio inayobeba ujumbe.

Sentensi ya kwanza

Hii huja mwanzo wa kifungu cha maneno. Hii inabeba ujumbe mzima wa kifungu cha maneno. Utaweza kujua kifungu kinahusu nini.

Mfano;

Kijiji changu ni maarufu kwa kuwa na mandhari nzuri na za kushangaza. Kwanza kinafahamika sana kwa kuwa na mlima Kilimanjaro ambao ni mrefu na mzuri. Pia upande wa pili kuna misitu na maua mazuri ya kupendeza sana. Mazingira haya mazuri yanafanya kijiji changu kuwa maarufu sana.

 lakini ningesema;  Mlima Kilimanjaro, upo kijijini kwangu na una mandhari nzuri, misitu na maua mazuri sana. Haya yangekuwa ni maelezo ya jumla jumla tu.

Sentensi ya maelezo

Sentensi hii inajibu swali lililoulizwa sentensi ya kwanza. Kwamba ni mandhari ipi hiyo ya kushangaza. Hivyo inatoa maelezo kuwa ni mlima Kilimanjaro , mrefu na mzuri. Sentensi za maelezo zinaweza kuwa 3-5 ikiwa maelezo yanayotolewa ni ya kina. Utaona sentensi inayoendelea inasaidia kutoa maelezo zaidi.

Sentensi ya kumalizia

Sentensi hii inajumuisha taarifa ambazo zimetolewa. Tazama tena kifungu cha maneno utaona sentensi hii

Mazingira haya mazuri yanafanya kijiji changu kuwa maarufu sana.

sio kila kifungu cha maneno kinaweza kuwa na sentensi hii. Hutumika zaidi ikiwa kifungu cha maneno ni kirefu na kuna haja ya kutoa majumuisho kwa ufupi.

Kifungu kamili cha maneno.

 Kijiji changu ni maarufu kwa kuwa na mandhari nzuri na za kushangaza. Kwanza kinafahamika sana kwa kuwa na mlima Kilimanjaro ambao ni mrefu na mzuri. Pia upande wa pili kuna misitu na maua mazuri ya kupendeza sana. Ni mlima volkeno mrefu kuliko yote barani Afrika. Una urefu wa mita 5,895 ni kama safu ndogo ya milima mitatu: Kibo, Mawenzi na Shira. Kibo ina theluji na barafuto ndogo kadhaa. Mazingira haya mazuri yanafanya kijiji changu kuwa maarufu sana.

 -RN-

waandishigroup@gmail.com

Kuandika kuna faida kwenye afya yako

Mara ya mwisho kuandika ilikuwa lini? siongelei kutumia simu au kifaa kama computer kuandika. Kama itakuwa ni muda unaweza kufikiri kufanya hivyo. Inaweza kuwa kutumia diary yako au note book . Hii ina faida mbalimbali kwenye mwili wako na akili. Hizi ni baadhi ya namna ambazo unaweza kufaidika nazo

Kuandika kwa mkono unaweza kujifunza kwa urahisi zaidi

Kutumia kalamu au penseli na daftari au kitabu cha kuandika kunakusaidia kuhifadhi sawasawa taarifa unazozihitaji hii inatokana na utafiti. Ndio maana wanafunzi ni muhimu wawe na madaftari. Akili ya binadamu imeumbwa iweze kusahau baadhi ya mambo. Hivyo kuandika kutakusaidia kuhifadhi taarifa zako muhimu na kuweka kumbukumbu.

Kueleza hisia kupitia maneno

Hili ndio maana ya lengo kuu la barua za urafiki. Wapo wanaoshindwa kuongea kwa sababu mbalimbali hivyo wanatumia barua na kueleza vile wanajisakia kwa wapendwa wao, kuwasalimia na kuwajulia hali. Hivyo kuwafanya wajisikie vyema kwa kutoa waliyonayo moyoni.

asante

Ni namna ya kushukuru kwa uliyotendewa

Mara moja kwa wiki au kwa mwezi kuna mtu aliyekufanyia jambo zuri. Unaweza kuandika kwa ajili ya kumshukuru. Mara nyingi Zaidi utakavyofanya hivyo watatambua kuwa umetambua jitihada zao na kuimarisha uhusiano wenu. Utajisikia vizuri zaidi kufanya hivyo maana ni jambo jema na sio kila mtu anaweza kushukuru.

Inasaidia mwili na akili yako kuwa sawa

Kuandika kwa kina kunasaidia kuwa na hali nzuri, ustawi, kupunguza msongo wa mawazo, kurekebisha shinikizo la damu na kusaidia mgonjwa kupona haraka. Kuandika kuelezea jinsi wagonjwa wanavyojisikia kunaongeza kasi ya wao kupona  pia kushirikishana na wengine kuhusu matatizo waliyoyapitia kumewasaidia sana,hasa kwa wenye unyanyapao, trauma, msongo mzito wa mawazo au uteja.

-RN-

Waandishigroup@gmail.com

VITU 5 VYA KUACHA ILI UFANIKIWE SANA

Habari za leo msomaji mpendwa. Natumai uko na afya njema na umekuwa na siku njema sana.  karibu tuwe pamoja kwenye makala hii. Mara nyingi, hutokea wakati ambapo umeweka malengo makubwa na unakuta unapotazama unaona kuwa sio hicho ulikuwa umepanga kufikia yaani ni kama paka anayejitazama kwenye kioo akaona yeye ni simba. Hii inahusiana sana na makala ya Vitu 7 unavyotakiwa kuacha haraka sana

Ukiona hali hiyo sio kwamba kuna vitu huvijui kwenye maisha yako. Hapana. Kuna vitu ambavyo inabidi uvitoe ambavyo umejifundisha.

  1. Akili ya muda mfupi. Kufikiri kwamba kuna jambo utalifanya kwa muda mfupi na kuona mafanikio ya haraka. Kuona kuwa wewe unaweza ukacheza bahati nasibu au kubashiri mchezo ukapata mamilioni, au kuingia kwenye michezo ya piramidi kama D9 ukatoka kimaisha. Watu waliofanikiwa ambao unawafahamu walikuwa na mipango mikubwa wakaiweka katika maeneo madogo madogo wakafanya kazi mpaka wakafikia malengo yao. Kuwa na ndoto kubwa na iweke kwenye mipango utakayoifanyia kazi kila siku. inaweza kuwa ni eneo la afya yako labda kufanya mazoezi, Inaweza kuwa ni uandishi, mradi au chochote kile. ona pia NGUVU YA MAWAZO YAKO
  2. Jimiliki. Hakikisha kila unachofanya kimetokana na maamuzi yako mwenyewe. Kamwe usiruhusu mawazo ya watu wengine bila kuyafanyia uamuzi wa mwisho. Chukua umiliki wa meli yako na wewe uwe nahodha na wala usiwe mhanga. Weka ndoto kubwa na hakikisha unakimbia mpaka kumaliza mbio, usiishie njiani. Wewe ni kondoo au simba?
  3. Acha visingizio. Wanaoshinda huwa wanajiuliza wanaweza kufanya nini. wanaoshindwa huwa wanajiuliza hawawezi kufanya nini. kwa mfano kama unalalamika hauna pesa ya kufanya jambo fulani. nikikwambia nakupa Bilion moja ukileta Milion kumi. hakika utafanya kila linalowezekana upate milioni kumi kwa sababu kila mmoja anatafuta namna ya kuwekeza. hivyo kukosa kwako fedha sio kisingizio fanya kazi zaidi.  
  4. Kupendwa. unahitaji kuusimamia ukweli. huhitaji kupendwa na kila mtu. hauwezi kumridhisha kila mtu hasa pale anapoingilia maamuzi yako. haijalishi mtu huyo ni nani kwako. anaweza kuwa mzazi, ndugu au mwenza. kama unalofanya ni jambo sahihi na halipingani na sheria za nchi. usiache mtu akurudishe nyuma. huna hata haja ya kuomba ruhusa. lifanye. wale wanaolipenda watakupenda  kwa jinsi ulivyo na kwa moyo wa dhati.
  5. Achana na wa kawaida. Tumia muda mwingi kwenye mambo yenye manufaa kwako kaa na watu ambao wameleta mabadiliko kwenye maisha yao. kaa na waliofanikiwa na utakuwa kama wao. mafanikio yako yanapimwa kutokana na rafiki zako watano walio karibu nawe. soma vitabu vya kukusaidia, blog za kukusaidia achana na televisheni na magazeti ya udaku. Pata mtu sahihi wa kukuongoza.

Twasiliane waandishigroup@gmail.com

‘Ni kitu gani cha kwanza ili uweze kuandika?’

Habari za leo.

Karibu waandishigroup, leo nina furaha sana, tangu nimeanza kushughulika na blogu hii nimetimiza mwezi mmoja.

Kama ungeniuliza swali. Ni kitu gani cha kwanza ili uweze kuandika?’

Kabla sijakujibu kuna usemi unasema ‘fanya vitu vya kwanza kwanza’  namaanisha kuwa kati ya vingi ulivyonavyo kuna ambavyo vinachukua nafasi ya kwanza kabla ya vingine. Hivyo katika uandishi kuna vitu ambavyo itabidi uvifanye kwanza kabla ya vingine.

Jibu ni rahisi kuliko unavyoweza kufikiri.  ‘anza kuandika’

Kuanza ndio somo gumu kabisa unaloweza kujifunza. Na ni rahisi kusema kuliko unavyoweza kulifanya.

Tatizo ni kwamba ubongo huwa unafanya kazi nzuri ya kukuletea sababu/ visingizio usifanye kitu fulani ambacho kinakupa changamoto na jinsi unavyozidi kusubiri ndio jinsi unajenga sababu nyingi za kutofanya jambo hilo.

Tangu mwezi uliopita nimefanyia kazi blogu hii ili kuwasaidia wale wanaoanza kuandika katika hatua zao za kujenga uwezo wao. Hakuna tena cha kukuzuia na milango ipo wazi kabisa.

Haijalishi kama una mawazo mengi na hujui wazo lipi ni bora kabisa, au hata kama huna wazo kabisa. Waandishigroup itakufanya ugundue ni upande upi uwe na kundi gani la hadhira.

Karibu tuendelee kuwa pamoja. Anza kuandika na anza leo. Nakupa wazo, andika unataka kuandika kuhusu nini na lengo lako ni nini. Umeona picha hapo juu, kuna watu wameamua kukimbia huku wamevaa suti. wengine wamevaa tai, wengine viatu vya moka. Huhitaji kuwa na kila kitu ili kuanza. Cha muhimu ni kuanza tuu.

NGUVU YA MAWAZO YAKO

Mawazo

Furaha

Mafanikio

Ustawi

Habari za leo napenda nikukaribishe kwenye makala nyingine ya waandishi group. Nafikiria sana kuhusu kufikiri, na ninafikiri unafikiri kuhusu kufikiria. Unajua nguvu iliyoko kwenye mawazo na jinsi inavyokuletea matokeo. Tafiti zimeonyesha kuwa katika mashindano kama vile bao, mpira wa miguu au mpira wa kikapu wale ambao wanakuwa na Imani kubwa ya kushinda mara nyingi ndio wao huwa wanashinda. Sio kwamba mara zote ndio inakuwa hivyo inaweza ikawa ni mashindano ya Ngumi na yule unayeona ana misuli Zaidi akapigwa na akashindwa.

Ndio hivyo hivyo pia kwenye mafanikio, yule ambaye anaamini kwamba anaweza kukamilisha jambo Fulani huwa ana nafasi kubwa sana ya kufanikiwa kwenye kile ambacho amepanga kukifanya. Kwa hiyo kinachotokea ni kuwa uchague mawazo yako au watu wengine wakuchagulie, au uache watu wengine wakuchagulie, mitandao ya jamii itakumbia nini cha kufanya, redio, magazeti, serikali, marafiki, majirani na wengineo lakini kama hautafikiria sawasawa kama hauchakati taarifa unazozipata na ukafanya maamuzi sahihi na kutoa hitimisho la msingi kwa kufikiri sawasawa  hapo utakuwa umeachia wengine wakutawale mawazo yako. Jambo moja muhimu ambalo unaweza kuelewa ni kuwa unapaswa kuwa na mawazo ambayo umefikiri wewe, uchague hicho ambacho umefikiria hapo ndipo furaha ya kweli na mafanikio ya aina zote yanafikiwa ni kwamba wewe umechagua mawazo yako. Halafu unayatawala au uwaachie watu au hali Fulani ichague mawazo yako, halafu mwazo yako yakutawale wewe.

Karibu waandishi group tukutane tena kwenye Makala nyingine. Kama umeona makala hii ni nzuri nakukaribisha uwaalike wengine kwenye jukwaa hili, ikiwa wanapenda kuandika nitawapa nafasi kwa utaratibu nitakaoweka hivi karibuni.

Vitu 7 unavyotakiwa kuacha haraka sana

Mara nyingi nimeandika Makala kuhusu vitu ambavyo unatakiwa kufanya, ila Makala hii naandika mambo ambayo nimuhimu UYAACHE ili uweze kuwa sawa. Tabia na vitendo ambavyo vitakufanya uwe na mahusiano mazuri. Nimejichunguza na kuona kuna mambo ambayo sikuwa nayafanya sawa sawa na ni muhimu niyaache

1. Usitafute uthibitisho

Wewe ni wa thamani. wewe ni wapekee. Na ukijichunguza rohoni unajua hilo. Usitafute uthibitisho kutoka kwa watu. Kama hujioni wewe ni wa thamani ndani ya roho yako ukiambiwa na mwingine haitakusaidia chochote. Angalia namna ya kuthibitishwa kwa matendo yako na sio kwa maneno ya wengine. Tambua mara nyingi watu sio wa kweli na hawatakwambia ukweli, watakusifia uongo ili ujisikie vizuri.

2. Acha kuomba msamaha hovyo

Kuomba msamaha ni jambo la muhimu sana. Na mara zote omba msamaha kwa jambo ambalo umelitenda. Kamwe usiombe msamaha kwa kuwa jinsi ulivyo. Usiombe msamaha kwa kutoa wazo.’’ samahani nina wazo’’ ‘’samahani nina swali’’ ‘’samahani napenda chumvi zaidi’’ kuna mtu alinifundisha hilo baada ya kumwambia ‘’samahani naomba niulize jambo’’ akaniambia huhitaji kuomba msamaha kwa hilo kama una swali wewe uliza moja  kwa moja. niligundua mara nyingi tunafanya hivyo wa sababu ya hofu. Fanya zoezi moja . wiki ijayo  hesabu mara ambazo umeomba msamaha bila sababu ya msingi. Ulikuwa kweli unaomba msamaha au ulikuwa na hofu?

3. Usijipandishe

Hii iko hivi, anakuja mtu anakueleza wazo, halafu wewe unakazana kumweleza jinsi ambavyo wazo hilo umelifanya kwa ubora wa juu kulio yeye. Sio kwamba inaonyesha inavutia Zaidi, hapana. Inaonyesha kwamba wewe unajionyesha. Unajisikia ni Zaidi ya wengine. Unaweza wakati mwingine usimaanishe hivyo. Lakini hivyo ndio hutokea. Sasa fanya hivi, kama ni jambo ambalo mtu anahitaji ushauri tafuta namna nzuri ya kumuelewesha.

4. Acha kukuza mambo

Karibia niandike acha kusema uongo . lakini nafikiri kukuza mambo ni tabia inayofanywa na watu wengi. Kama umekuza mambo kwa ajili ya kuandika hadithi hilo sio ninalo zungumzia hapa. Ninazungumzia umbea na kuwapa watu hofu na kusema mambo ambayo uhalisia wake sio kama unavyoeleza. Utasikia mtu anasema ‘’hii kazi itaniua’’ mmh kweli?  ‘’Yaani nimechoka hadi nasi kia kufa kufa’’ mmh!

5.Hali ya kusita sita

Nilikuwa kwenye mkutano Fulani mtu akasema ‘’kuna jambo moja ni muhimu ila bado sina uhakika nalo’’ . hali hii ni mbaya kwa sababu bado hujawa na uhakika na hicho unachotaka kusema kimekaa sawasawa. Ni bora usiseme chochote kuliko kutoa taarifa ambazo haziko tayari

6. Kujishusha Zaidi

Umewahi kupigiwa simu mtu anakuomba fedha ana shida halafu hutaki kumpa halafu unaanza kumueleza shida Zaidi kuliko alizonazo? Hicho ndio ninakiongelea. Au mtu anakwambia amepata shida Fulani halafu wewe unamwonyesha wewe ni mbaya Zaidi. Unaweza kumwambia mtu unaelewa hali aliyonayo. Labda pengine anataka faraja tuu ila sio kujishusha Zaidi.

7. Kuigiza

Huhitaji kuigiza, wala kuishi maisha ambayo wewe sio. Kama unaigiza jiulize unafanya hivyo wakati gani? Je ni wakati uko na watu Fulani? Kwa nini usione kwamba umetosheleza? Usiende mahali ambapo unajisikia kukaa kama unaigiza. Unapoigiza unakosa nafasi ya kuungana na watu. ila ukiwa halisi unapata watu wa kuungana nao, watu watakuheshimu na utaonyesha umiliki. Maigizo ni kwa sababu ya kuona kwamba hauna thamani hivyo unaigiza ili upendwe, usifiwe, uonekane daraja la juu. Leo nakwambia kuwa wewe ni wa thamani sana.